Maombi ya Kupandisha Ada Yatinga Wizarani - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Wednesday, 23 December 2015

Maombi ya Kupandisha Ada Yatinga Wizarani

Shule nyingi za msingi na sekondari zisizo za Serikali, zimetuma maombi kwa Kamishna Mkuu wa Elimu nchini kuomba kibali cha kupandisha ada katika mwaka ujao wa masomo.

Hatua hiyo ni kuitikia amri ya Serikali ya kuzipiga marufuku shule binafsi, kupandisha ada kiholela na badala yake shule zote zinatakiwa kuwasilisha maombi ya kupandisha ada hiyo mpya kwa kamishna huyo ili yajadiliwe.

“Kwa kweli baada ya tangazo lile shule nyingi zimeleta maombi yao hapa na kilichobaki ni kwa kamishna wa elimu kuhakikisha anapitia maombi hayo kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vilivyowekwa na Serikali,” alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Sifuni Mchome .

Alisema lengo la maombi hayo ni kuondoa tabia ya wamiliki wa shule zisizo za Serikali, kupandisha ovyo ada kwa kadiri wanavyotaka, jambo lililosababisha shule nyingine kugeuza elimu kuwa biashara badala ya kutoa huduma.

Lengo la wizara hiyo ya kutaka maombi hayo na kiwango cha ada wanazotoza kwa sasa ni kubaini shule, ambazo zinafanya biashara na zile ambazo zinatoa huduma ya elimu kwa kuisaidia Serikali. Shule ambazo zitabainika kufanya biashara, zitatakiwa kulipa kodi kutokana na biashara hiyo wanayoifanya.

Profesa Mchome aliwataka wazazi kuisaidia Serikali kwa shule ambazo hazitafuata utaratibu huo, watoe taarifa kwa halmashauri za wilaya, wizarani ili kuhakikisha zile ambazo zimekaidi agizo hilo, zinachukuliwa hatua.

“Hizi shule ni nyingi ziko zaidi ya 1,000, naomba wazazi watusaidie kwa shule ambazo zitakaidi agizo la Serikali watuletee taarifa ili tuweze kuchukua hatua kwa shule husika,” alisema Profesa Mchome ambaye alisisitiza kuwa wazazi wafanye vikao na shule husika kuhusu upandishwaji ambao unatangazwa na shule husika.

Alisema maombi ya kupandisha ada ambayo yanawasilishwa kwa Kamishna wa Elimu, yanaweza kukubaliwa au kukataliwa kulingana na hoja mbalimbali ikiwemo ukubali wa wazazi baada ya kufanya kikao cha uongozi wa shule, huduma inayotolewa na shule husika.


Nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa upatikanaji wa elimu unaendana na uwezo wa wananchi na viwango vilivyokubaliwa.
Post a Comment