Dr. Ndalichako Aahidi Mapinduzi ya Elimu Nchini......Aapa Kupandana na Ukosefu Wa Madawati, Chanzo Cha Kuzorota Elimu na Wanaopandisha Ada Kiholela - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Tuesday, 29 December 2015

Dr. Ndalichako Aahidi Mapinduzi ya Elimu Nchini......Aapa Kupandana na Ukosefu Wa Madawati, Chanzo Cha Kuzorota Elimu na Wanaopandisha Ada Kiholela


WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Joyce Ndalichako, amesema atafuatilia shule za Serikali ili kujua sababu za kufanya vibaya katika mitihani yao. 
 
Dk Ndalichako ambaye aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), amesema hayo jana baada ya kuapishwa na Rais John Magufuli, kushika wadhifa huo.

“Kwa kuwa lengo langu ni kuona elimu bora inatolewa, nitafuatilia kujua sababu ya shule maalumu za Serikali kushuka kiwango chake katika ufaulu wa mitihani,” alisema. 
 
Kwa mujibu wa Dk Ndalichako, shule hizo za Serikali hasa za vipaji maalum, ndizo awali kila mwanafunzi alipenda kwenda kusoma tofauti na sasa ndio maana anataka kujua kulikoni.

Shule hizo ni pamoja na Mzumbe, Ilboru, Tabora Wavulana, Tabora Wasichana, Kilakala na Msalato.

Wanaoongeza Ada Kiholela Kukiona
Kuhusu upandaji holela wa ada za shule binafsi, Dk Ndalichako alisema atapambana na vyuo vikuu na shule binafsi, zinazofanya ujanjaujanja wa kupandisha ada tofauti na ile iliyoandikwa kwenye barua za kuwaita wanafunzi, jambo linalosababisha usumbufu kwa wazazi.

Alisema lengo lake ni kuhakikisha Tanzania inatoa elimu bora kwa wahitimu wa vyuoni na sekondari, itakayowawezesha kukidhi soko la ajira la kimataifa.

Pamoja na ubora huo, Dk Ndalichako alisema ataangalia uwepo wa miundombinu kwa wanafunzi wa kuanzia shule ya msingi na sekondari, ambako alikiri kuwa baadhi ya wanafunzi wanaketi chini na wengine wana matatizo ya mashimo ya vyoo.

“Inakuwaje shule yenye maelfu ya wanafunzi watumie shimo moja la choo, haya na mambo mengine yanakwaza wanafunzi wasipende shule na wengine wakatize masomo yao. 

“Tunataka kuandaa mwanasayansi, hivi kweli mwanafunzi anayeketi chini anaweza kuwa mtaalamu mzuri wa sayansi? Ni lazima tuwezeshe shule zetu ziwe na miundombinu rafiki kwa wanafunzi,” alisema Dk Ndalichako.


Pia alisema atashughulika na tatizo la baadhi ya vyuo kutoa kozi zinazoenda kinyume na ithibati walizopewa na mamlaka za elimu, jambo linalofanya wanafunzi wanaosoma kwenye vyuo hivyo kutotambuliwa na waajiri.
Post a Comment