Mgombea Urais wa ACT-Wazalendo Aahidi Kumteua Magufuli Kuwa Waziri wa Ujenzi - LEKULE

Breaking

8 Oct 2015

Mgombea Urais wa ACT-Wazalendo Aahidi Kumteua Magufuli Kuwa Waziri wa Ujenzi



Mgombea urais kupitia ACT-Wazalendo, Anna Mghwira amesema akipata ridhaa ya wananchi kuwa rais wa Tanzania, atamteua mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kuwa Waziri wa Ujenzi.

Akizungumza kwenye mkutano wa kuhitimisha kampeni zake kwa Mkoa wa Arusha, mgombea huyo alisema Dk Magufuli ni mtendaji ndiyo maana anasisitiza kujenga madaraja na barabara kila anakokwenda.

“Kazi ya rais si kujenga barabara, sasa kwa kuwa yeye yuko vizuri katika suala la ujenzi nichagueni niwe rais wenu ili nije kumchagua aendelee kujenga barabara, kazi anayoifanya kwa ufanisi,” alisisitiza.

Awali, katika mikutano aliyofanya katika majimbo ya Arumeru Magharibi, Arumeru Mashariki na Arusha Mjini, mgombea huyo alisema Serikali yake ina sera mahsusi kwa ajili ya wananchi wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.

Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa yenye utajiri mkubwa nchini ukiwa umezungukwa na rasilimali mbalimbali.

Alisema mkoa huo pekee wenye madini ya Tanzanite nchini na duniani kwa ujumla, pia una mbuga mbalimbali za wanyama.

Kwa upande wa kilimo, alisema mazao kama kahawa, maua, vitunguu maji na mbogamboga ni vipaumbele vyake.

“Tunataka Watanzania wajiwekee akiba ili tutunishe mifuko ya hifadhi ya jamii. Katika utawala wetu tunataka watu milioni tano waingie kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kipindi cha mwezi mmoja,” alisema na kuongeza:

“Ukiweka Sh10,000 Serikali itakuongezea Sh20,000, hivyo kila mwezi utakuwa na uhakika wa kuingiza Sh30,000,” alisema.

Alisema mfumo wa maisha ya Watanzania unahitaji kufanyiwa mabadiliko na wao ndio wanaopaswa kusimamia suala hilo.

No comments: