LOWASSA: Kesheni Vituoni Mkilinda Kura Zenu Zisiibiwe Maana Wenzetu ni Wataalam Sana wa Kuiba - LEKULE

Breaking

8 Oct 2015

LOWASSA: Kesheni Vituoni Mkilinda Kura Zenu Zisiibiwe Maana Wenzetu ni Wataalam Sana wa Kuiba



Wakati leo akitarajiwa kuhutubia mkutano wa kampeni jiji Arusha, mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amewataka Watanzania kukesha vituoni wakilinda kura zisiibiwe.

Lowassa aliyasema hayo jijini Arusha jana, alipopita eneo la Ngaramtoni, Jimbo la Arumeru Magharibi na kuzungumza na wananchi kabla ya kuendelea na ziara yake kwenye Jimbo la Longido na Namanga.

Kauli ya Lowassa ilitokana na kelele za wananchi waliokuwa wakiimba ‘rais, rais…’.
 
“Natamani hizo kelele zingenipeleka Ikulu, kitakachonipeleka Ikulu ni kura, nahitaji kura nyingi, hakikisheni mnapiga kura na kukesha vituoni mpaka mpate matokeo, wale wenzetu ni maarufu kwa kuiba kura,”alisema.

Alisema Mkoa wa Arusha una historia na Chama cha TANU pamoja na CCM, kwani ndipo lilipozaliwa Azimio la Arusha, lakini mwaka huu wataachana na chama hicho.

“Nimeona (CCM) wakipitapita Monduli na Arusha, nawaambia wasubiri tarehe 25, huu ndio mwaka wao wa kutoka madarakani… siku ikifika nendeni na vichinjio vyenu mkawakate,” alisema Lowassa.

Akizungumzia kero ya maji eneo hilo, alisema wakati akiwa Mbunge wa Monduli alichukua maji na kuyapeleka, huku akiwapa miundombinu viongozi wa Arumeru ili wapeleke maji kwa wananchi wao, lakini wakashindwa.

“Kulikuwa na pampu nne, mbili zikapeleka maji Monduli, mbili nikawapa viongozi wa Arumeru ili walete maji, tena niliwapa bure hizo pampu, sasa mimi nifanye nini zaidi ya hapo?” alisema. Alisema akipata madaraka atashughulikia suala hilo na litakuwa historia.

Akiwa Longido, Lowassa alisema ameamua kuwania urais kwa sababu ana hasira na kumaliza umasikini, kwani siyo mpango wa Mungu watu wawe masikini.

“Nina usongo na umasikini, umasikini siyo mpango wa Mungu… nia yangu ni kuongoza taifa hili ili kuondokana na umasikini, nitaanza na elimu ambayo yote italipiwa na Serikali.

“Jambo la pili litakuwa kilimo, wakulima wataruhusiwa kuuza mazao popote na hawatakuwa na ushuru wowote kwenye mazao yao,”alisema.

Aidha, alisema anashangaa watu ambao wanazunguka na kumtukana wakati yeye hawajibu.

“Nikiwajibu wanaozunguka na kunisema vibaya, watu watashindwa kutofautisha mjinga na mwerevu,” alisema. 
  
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, aliwataka wananchi wanapokwenda kupiga kura waende na kalamu zao.
  
 “Jamani nawaomba mnapokwenda kupiga kura, mwende na kalamu zenu kwani tuna wasiwasi na mambo fulani,” alisema.

Akiwa Namanga, alisema akiingia madarakani ataendeleza ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuhakikisha raia wa nchi hizo wanafaidi wote.

“Mimi na Serikali yangu, nikishinda tutaendeleza ushirikiano wa Afrika Mashariki, mpakani hapa siyo magari yanasimama simama, kazi ifanyike bila vikwazo, Namanga mtu akitaka kupita siyo asumbuliwe,”alisema.

No comments: