Chopa ya CCM Yazua Kizaa zaa Mazishi ya Mtikila - LEKULE

Breaking

9 Oct 2015

Chopa ya CCM Yazua Kizaa zaa Mazishi ya Mtikila


Kada wa chama cha Mapinduzi ambaye pia ni mgombea ubunge wa jimbo la Ludewa mkoani Njombe jana aliwasili kwa chopa kwenye mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Siasa cha DP Mchungaji Christopher Mtikila.

Wakati chopa hiyo inatua katika eneo la Msiba wananchi waliacha kusikiliza Salam mbali mbali za viongozi na kukimbilia kutazama ili kufahamu ni nani aliyekuwemo ndipo alipoteremka Mgombea Ubunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe.

Mazishi ya Mchungaji Mtikila yalihudhuriwa na viongozi kadhaa wa serikalini akiwemo Msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Mutungi, mkuu wa mkoa wa Njombe Dr. Rehema Nchimbi ,wanasiasa pamoja na ndugu na jamaa kutoka sehemu mbalimbali nchini Tanzania.

Akizungumza katika mazishi hayo Filikunjombe alisema mbali ya ukorofi wa Mtikila kwa kile alichokiamini ila kwake alikuwa ni mshauri mkubwa wa Ubunge wake katika jimbo la Ludewa.

Filikunjombe alisema katika kuamini kwake na kusimamia anachokiamini hadi umauti unamkuta alikuwa akitetea kuwepo kwa nchi ya Tanganyika na ndio maana kazikwa na bendera ya Tanganyika na kudai kuwa hakuna kosa kupigania Tanganyika kwani Tanganyika inahitajika.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dr. Rehema Nchimbi alisema kuwa Mkoa wa Njombe umepoteza kiongozi makini na kuwa katika kumuenzi ni vema kwa vyama vya siasa kuendesha kampeni za amani na utulivu  kuwa hivisasa taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu.


Kwa upande mwingine Naibu Katibu mkuu wa DP Taifa Abdul Mluya alisema kuwa suala la kifo cha mwenyekiti wake ni utata mtupu na bado wanaendelea kuchunguza.
Filikunjombe akitoa salamu zake wakati wa mazishi ya Mtikila
Mkuu  wa mkoa wa Njombe Dr Rehema Nchimbi kulia akiwa na Deo Filikunjombe mgombea  ubunge jimbo la Ludewa na mbunge aliyemaliza muda  wake, katikati kushoto ni msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mutungi jana  wakati wa mazishi ya Mchungaji Mtikila
Mjane  wa Mtikila  akiweka shada la maua 

No comments: