.Ukawa: NEC inatuvurugia mipango majimboni - LEKULE

Breaking

3 Jul 2015

.Ukawa: NEC inatuvurugia mipango majimboni

Dar es salaam.
Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ameishukia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kushindwa kutangaza mgawanyo wa majimbo, akisema kuchelewa huko kunavuruga mipango yao.
Ukawa, inayoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, imekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais hadi diwani na viongozi wa vyama hivyo wameshakutana mara kadhaa kuzungumzia kugawana majimbo kulingana na nguvu ya chama kwenye eneo husika.
Hata hivyo, vimeshindwa kumalizia kazi hiyo kutokana na kutokamilika kwa mgawanyo wa majimbo kama NEC ilivyoahidi Mei 12 kuwa majimbo mapya kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 yangetangazwa Juni 30.
Akizungumza jana, Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema aliitupia lawama NEC akisema wakati huu ilitakiwa kuwa imeshamaliza suala la majimbo na kushughulikia mambo mengine.
“Tunataka kutengeneza ratiba ya mpango kazi, lakini tunashindwa. Tunataka tujue majimbo mapya ili twende huko, lakini sasa tunashindwa na muda unakwenda,” alisema Mbowe.
Akizungumzia ukimya wa kutangaza majimbo hayo licha ya kusema ingefanya hivyo Juni mwishoni, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema hadi sasa Tume hiyo haijakamilisha ugawaji wa majimbo lakini bado wanaendelea na mchakato huo.
Alisema Tume yake imeamua kugawa majimbo hayo kwa kuzingatia vigezo mbalimbali, ikiwamo idadi ya watu, upatikanaji  wa mawasiliano, hali ya kijiografia na kanuni za uchaguzi wa Rais na wabunge za mwaka 2010.
Jaji Lubuva pia alisema Tume itayagawa majimbo hayo kwa kuzingatia uwepo wa miundombinu bora, hali ya kiuchumi kwa kuweka uwiano kati ya eneo moja na jingine, mawasiliano ya simu na vyombo vya habari kwa ajili ya kupata mwakilishi atakayeharakisha maendeleo katika eneo husika.
Wakati ikisuasua kutangaza majimbo mapya ya uchaguzi, NEC pia inakabiliwa na kibarua kingine cha kumalizia uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Kazi hiyo imekumbwa na matatizo kadhaa na inatakiwa ikamilishwe katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, lakini imeahirishwa kutokana na kuchelewa kwa mashine zinazotumika za teknolojia ya mfumo wa kuchukua alama na taswira za mpigakura (Biometric Voters Registration).

Jaji Lubuva alisema kuwa kuna baadhi ya majimbo ambayo ni makubwa, jambo ambalo alisema linatokana na ongezeko la watu nchini.

Ugawaji wa majimbo unatakiwa kufanyika mara kwa mara au angalau mara moja baada ya miaka 10.

“Ugawaji wa majimbo ulifanyika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kwa kuwa sasa tunaelekea uchaguzi mwingine, lazima tufanye hivyo,” alisema  Jaji Lubuva.

Kauli ya Mbowe

Akizungumzia kusuasua huko kwa ugawaji majimbo, Mbowe alisema NEC inataka ifanye mambo mengi kwa wakati mmoja.

“Tume imezidiwa na majukumu; inataka kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, huku muda ukiwa haupo. Kila siku wanaahirisha hili mara lile na mengine hawayatolei taarifa,” alisema Mbowe.

Alisema tangu Tume hiyo ilipotangaza kugawa majimbo ya uchaguzi nchi nzima, bado mpaka leo haijafanikisha shughuli hiyo, jambo ambalo linasababisha kuchelewa kwa umoja huo kugawana majimbo.

“Uchaguzi ni vita,” alisema Mbowe. “Sasa sijui wanasubiri nini? Mpaka leo hawataki kutangaza hayo majimbo waliyosema wanayagawa, sisi tunasubiri wakimaliza tu tunaanza mchakato wa kugawana ila kwa hali ilivyo sasa, hatuwezi kufanya lolote.”

No comments: