Nyumba ya mwandishi wa Nyerere yauzwa kinyemela - LEKULE

Breaking

3 Jul 2015

Nyumba ya mwandishi wa Nyerere yauzwa kinyemela

Dar es Salaam.
Nyumba ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Mwalimu Julius Nyerere, Paul Sozigwa imeuzwa katika mazingira ya kutatanisha na mke wake Monica Kuga baada ya mwanahabari huyo kupata maradhi ya kupoteza kumbukumbu.
Kuga aliiuza  nyumba hiyo kwa Mahamood Duale kwa Sh600 milioni mwaka 2010, huku watoto wake wanne wa Sozigwa wakipinga uuzwaji huo wakidai kuwa baba yao aliwakabidhi nyumba hiyo mwaka 1998.
Mtoto wa mwisho wa Sozigwa ambaye pia ametajwa kama msimamizi wa mirathi, Moses alisema wana vielelezo vya wosia aliowaachia baba yao akiwa Finland kabla ya tatizo lake la kupoteza kumbukumbu halijawa kubwa.
“Tulirekodi kila kitu na ushahidi wa maandishi upo, baba alisema nyumba ile ni ya watoto na siyo yake wala ya mke wake. Lakini pia tulirekodi sauti yake, tunashangaa kwanini mama ameiuza,” alisema Moses.
Kwa maelezo ya wanafamilia hao, Kuga aliachana na Sozigwa mwaka 1974 na kufungua kesi ya kudai talaka mahakamani jambo ambalo baba yao alilipinga.
“Alitaka kuachana na baba tena sisi tukiwa wadogo ili wagawane mali, lakini baba hakukubali, tunashangaa iweje leo arudiane naye halafu auze nyumba?” alihoji Moses.
Moses alieleza kuwa mama yao alimchukua Sozigwa na kuishi naye kama kisingizio cha kujihalalishia  uuzwaji wa nyumba hiyo iliyopo maeneo ya Kurasini, karibu na shule ya Sekondari ya Jitegemee.
“Mama alimkana baba na wameachana kwa miaka zaidi ya 34 na aliidai talaka hadi mahakamani kwa nguvu, halafu baba alipoanza kuumwa anadai anataka kumlea kumbe ni ujanja wake  tu, alitaka kuuza eneo la familia,” alidai mtoto huyo.
Kwa mujibu wa wanafamilia hao, Kuga alighushi hati ya nyumba hiyo na kuiuza kwa Duale lakini baadaye aliwataka wampe hati halisi ili amkabidhi Duale.
Lakini baada ya kuona kuwa hawezi kuipata, kwa kushirikiana na Duale walianza kumsumbua Moses na hatimaye walimfungulia kesi mahakamani.
Hata hivyo, baada ya Duale kuzungumza na wakili wa familia ya Sozigwa, aliambiwa ukweli kuwa hiyo nyumba ina utata wa wanafamilia hali iliyomsababishia Duale mshtuko hadi kupooza.

“Huyu Duale alizungumza na wakili wetu, akaambiwa ukweli kuwa asinunue hiyo nyumba kwa kuwa haina hati na alipoonyeshwa hati halisi alishtuka na kupata kiharusi kwa sababu alikuwa ameshalipa fedha zote,” alisema Moses.

Akiendelea kusimulia, Moses alisema mauzo ya nyumba hiyo yana utata na kuna dalili ya rushwa kwani yameidhinishwa na baraza la ardhi la Wilaya ya Temeke ambalo kwa kawaida, lina haki ya kuidhinisha mauzo ya nyumba yenye thamani ya Sh50 milioni na chini ya hapo, wakati thamani halisi ya nyumba hiyo ni Sh900 milioni.

“Tunashangazwa na kitendo cha mama kuuza nyumba hiyo kwa Sh600 milioni wakati tathmini iliyofanywa mwaka 2010 ilionyesha kuwa ina thamani ya Sh900 milioni,” alisema Moses.

Moses ambaye alizungumza kwa niaba ya ndugu zake watatu, Salome, Irene na Ephata alisema licha ya mama yao kuuza nyumba kwa mamilioni ya fedha lakini alikataa kusaidia kutoa fedha za kumpeleka baba yao nchini Finland kwa matibabu. “Ilitubidi kutembeza bakuli hadi kwa Rais Jakaya Kikwete ili tupate msaada wa matibabu ya mzee,” alisema.

Mwananchi lilizungumza na Kuga ambaye alisema anawashangaa watoto wake kwa kushindwa kujua sheria zinavyofanya kazi na kuanza kumrushia tuhuma zisizo na ukweli kuwa ameuza nyumba kwa ujanja.

“Hii kesi imeenda mahakamani  hadi mahakama kuu na nimeshinda mara tatu, lakini hawa wanaona kuwa wao ndiyo wana haki ya nyumba ambayo mimi na baba yao tuliijenga, wanakata rufaa kila siku,” alisema. Alieleza pia sababu za kuishi na Sozigwa licha ya kuwa walitengana kwa zaidi ya miaka 34.

Alisema baada ya kuona hali ya mumewe huyo siyo ya kuridhisha aliamua kurejea kumtunza na siyo kwa ajili ya nyumba. “Nilimhurumia mzee nikaamua kuishi naye ili nimlee na ndiyo hapo tulipokubaliana naye tuiuze nyumba,” alisema.

Kuga ambaye aliwahi kugombea ubunge wa Temeke kwa tiketi ya DP mwaka 1995, alisema watoto wake hao walifikia hatua ya kuficha hati halisi ya nyumba hiyo ili kuzuia uuzwaji.

Lakini hata hivyo, Kuga alisema yeye na wakili wake walitoa matangazo kwenye magazeti kuwa hati hiyo imepotea ili kupata kibali kutengeneza hati mpya ili waweze kuiuza nyumba hiyo.

“Hali ya baba yao ni mbaya lakini naona na hawa watoto hali yao ni mbaya zaidi kwa sababu hawajui kitu wanachokifanya; nyumba ni yetu mimi na mzee wao kinawauma nini? Alihoji.

Kadhalika Kuga alisema mpaka sasa Duale tayari ana hati na ameshakuwa mmiliki kamili wa nyumba hiyo.

No comments: