LOWASSA CHADEMA: Fitina zimempeleka Lowassa upinzani - LEKULE

Breaking

29 Jul 2015

LOWASSA CHADEMA: Fitina zimempeleka Lowassa upinzani

Hatimaye waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa amekitosa chama chake cha CCM na kutua Chadema. Huko ndiko anatarajia kuendelea na safari yake ya matumaini aliyoianza na sasa anatarajiwa kupambana na ikiwezekana kukidhoofisha chama kilichomlea katika harakati za kuingia Ikulu.
Serikali ya CCM ilimpa fursa nyingi za uongozi kuanzia ukurugenzi katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC) na uwaziri. Amewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sheria na Bunge 1990–1993), Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi (1993–1995), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Umaskini 1997–2000), Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo (2000–2005) na Waziri Mkuu (2005–2008).
Alipata kila aina ya msaada aliouhitaji, akawa na nguvu za kiutendaji, kudhoofisha upinzani katika jimbo lake na hata kuthubutu kufanya maamuzi magumu katika nafasi mbalimbali alizoshika. Lakini baada ya kufanyiwa fitina wakati wa mchakato wa kuteua mgombea urais kupitia CCM, mbunge huyo wa Monduli tangu 1990 ameamua kuungana na wapinzani kuitia adabu CCM.
Lowassa atakuwa kada wa tatu mwenye nguvu kuitikisa CCM na kuidhoofisha katika baadhi ya maeneo. Makada wengine waliowahi kuitesa CCM, kwa upande wa Bara ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Mrema; na kwa Zanzibar aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi, Seif Sharrif Hamad.
Je, Lowassa ataujenga upinzani? Je, anaingia Chadema peke yake au pamoja na mafuriko ya watu waliokuwa wanakanyagana kumdhamini alipokuwa anagombea urais kupitia CCM? ni maswali ya msingi kujiuliza. Makada kadhaa wamewahi kujiondoa CCM na kujiunga na upinzani lakini yeye anakuwa kada wa kwanza aliyewahi kuwa waziri mkuu kukihama chama tawala

Mrema ndani ya NCCR

Upinzani dhidi ya chama tawala nchini una historia ndefu. Kada wa kwanza kupinga sera za chama tawala ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Oscar Kombona enzi za Tanu na kwa kuwa mfumo wa vyama vingi uliharamishwa mwaka 1965, alikosa sehemu ya kupumulia hivyo alikimbilia uhamishoni, Uingereza.
Miaka ya 1980 waliibuka wanaccm kadhaa waliotaka mabadiliko, akiwamo mwasisi wa Chama cha Wananchi (CUF), James Mapalala. Harakati zake zilihesabika kuwa uhaini hivyo watu waliogopa kujiunga naye hasa walipomwona akikamatwa na kuwekwa kizuizini mara kwa mara.
Miaka ya mwanzoni mwa 1990 akajitokeza Mrema. Kwanza, alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu, alikuwa kizuizi cha mageuzi.
Pamoja na vigingi hivyo, mwaka 1991 wanaharakati walianzisha vyama vya kiharakati. Mapalala alianzisha Chama cha Wananchi na wengine kama Mabere Marando wakianzisha National Committee for Constitutional Reforms (NCCR) ambayo baadaye iligeuzwa kuwa chama cha NCCR-Mageuzi.
Waanzilishi waliotoka CCM walikejeliwa kwa kuitwa majina kama vibaraka waliotumwa na mataifa makubwa kuisambaratisha nchi; malaya tu wa kisiasa. Pia walifananishwa na mchwa ambao watakufa kwa jua kali kwenye mwamba.  Haikutosha.
Siku Mrema alipotembelea kwa helikopta wilaya ya Namanyere, Rukwa na kukuta imesimikwa bendera ya NCCR, alirejea Dar es Salaam na mikakati ya kuiangamiza kabla haijawa tishio.
Baadhi ya wajumbe wakashawishiwa kujiondoa waanzishe vyama vyao ili NCCR idhoofike. Ikawa hivyo, mmoja aliasisi UMD huku waliobaki waliibadilisha NCCR na kuunda chama kwa jina la NCCR-Mageuzi, kikipewa maana ya National Convention for Construction and Reform yaani Chama cha Mageuzi na Ujenzi wa Taifa.
Baada ya upinzani kuruhusiwa rasmi Julai 1992 vikasajiliwa vyama vingine kama DP, FORD, NLD, NRA, PONA, Tadea, UPDP, CUF, Chadema, TLP, na UDP na vingine vinaendelea kusajiliwa.
Pili, mambo yalipokuwa magumu serikalini Mrema aliitosa CCM na kuipaisha NCCR alipojiunga nayo mwaka 1995 na akateuliwa kuwa mgombea urais.
Mrema alipeleka mawimbi mazito CCM lakini kwa vile hakuwa na mtaji wa wanaccm aliohama nao, kura hazikutosha kumwezesha kuongoza nchi. Hata hivyo, aliingiza wapinzani kadhaa bungeni miongoni mwao ni waliojiondoa CCM kama Steven Wassira (Bunda), Makidara Mosi (Moshi Mjini), Dk Masumbuko Lamwai (Ubungo),
Wengine ni Thomas Ngawaiya (Moshi Vijijini), Festus Limbu (Magu), MwinyiHamisi Mushi (Siha), James Mbatia (Vunjo), Paulo Ndobho (Musoma Vijijini), Mfalamagoha Kibasa (Iringa Mjini), Marando (Rorya) na wengineo.

Mapalala na Hamad

Baada ya Mapalala kukutana na viongozi wa chama cha Kamahuru ya Zanzibar kuunda Chama cha Wananchi (CUF), hakudumu, aliondolewa baada ya kutokea kutoelewana na wenzake. Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharrif Hamad ndiye alibaki kuwa nguzo imara ya chama hicho na kutikisa kuta za CCM visiwani Zanzibar.
Kama ilivyokuwa kwa Mapalala, Maalim Seif amepitia masahibu mengi ya kutisha lakini yu imara hadi leo. Alipokuwa CCM alikuwa madhubuti, kiongozi mwenye mvuto na aliyeamini katika misingi.
Hata hivyo, uamuzi wake wa kuwania urais wa Zanzibar kupambana na Mzee Idrid Abdul Wakil uliwachefua CCM. Wakamfitinisha. Januari 1988 alitemwa kwenye Baraza la Mapinduzi na akavuliwa cheo cha Waziri Kiongozi. Mei 1988 akafukuzwa uanachama wa CCM pamoja na wenzake sita kutoka Baraza la Wawakilishi. Mei 1989 alitiwa mbaroni na akafunguliwa kesi kwa madai ya kukutwa na nyaraka za siri za Serikali. Tangu mwaka 1989 hadi 1991 alikuwa mahabusu ya Polisi Zanzibar.
Pamoja na mateso hayo, Maalim Seif amejenga upinzani wa nguvu Zanzibar na kuitokomeza CCM kisiwani Pemba akishirikiana na makamanda kadhaa baadhi wakiwa ni waliowahi kukabiliwa na kesi ya uhaini kama  Zulekha Ahmed Mohamed, aliyewahi kuwa naibu waziri wa Fedha Tanzania, Hamad Rashid Mohamed, Machano Khamis Ali, Hassan Mbarouk Hassan, Mohamed Ali Maalim, Shariff Haji Dadi, Ramadhan Shamna Abdi, Soud Yusuf Mgeni, Said Zam Ali, Pembe Ame Manja, Abbas Zam Ali, Nassor Seif Amour, Abdallah Said Abeid na Zeina Juma Mohamed.
Baadhi ya makada wa zamani wa CCM wanadai kuwa Maalim Seif hajawahi kushindwa katika chaguzi za Zanzibar, japokuwa hajaachiwa ikulu. Nguvu yake ilisababisha kubadilishwa katiba ili chama chake kishirikishwe katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Kwa upande wa Bara, CUF ilipata wafuasi wengi akiwamo Mwenyekiti, Prof Ibrahim Lipumba aliyerithi mikoba ya Musobi Mageni. Mwaka 2000 na 2005 amewahi kushika nafasi ya pili katika mbio za urais.

Safari ya Lowassa

Kwa wiki tatu sasa upepo wa siasa umekuwa ukivuma kwa Lowassa aliyetawala siasa za hapa nchini tangu mwaka 2008 alipojiuzulu nafasi ya waziri mkuu kutokana na kuhusishwa na kashfa ya kampuni isiyo na uwezo wala mtaji ya Richmond kupewa zabuni ya kufua umeme wa dharura nchini.
Kamati Maalumu ya Bunge chini ya Mwenyekiti, Dk Harrison Mwakyembe ilifanya uchunguzi wa kina na kuwasilisha ripoti bungeni kwamba kulikuwa na mkono wa Lowassa katika utolewaji wa zabuni hiyo. Serikali inasema aliwajibika kisiasa.
Lowassa hakuwa na neno alipokatwa kuwania urais mwaka 1995 lakini mazingira yaliyojitokeza ya kukatisha safari yake ya ikulu mwaka huu yamezua nongwa na kuteka siasa za nchi kwa wiki tatu sasa.
Waliomkata wamekuwa wakihaha, bila mafanikio, kumsihi asihame chama. Amepuuza na ameamua kuondoka, tayari amepokewa na Ukawa ambao wanatarajia kumteua kugombea urais kupambana na mgombea wa CCM, Dk John Magufuli.
Safari yake ya matumaini ni kuishi ikulu. Matarajio ya Ukawa ni kupanga ikulu. Matarajio ya Watanzania ni kupata mabadiliko nje ya CCM. Ikiwa Lowassa atamega nusu ya wanachama na mashabiki wa CCM, chama hicho tawala kitaanza kuonja joto ya jiwe na kuwa chama pinzani.

Dk Slaa na Dk Kabouru

Watu wengine waliowahi kuhama CCM ni mwasisi wa Chadema aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Edwin Mtei na wanasiasa wengine kama Bob Makani. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ambaye mwaka 1995 alishinda kura za maoni ndani ya CCM katika jimbo la Karatu, lakini wenye chama walimtosa wakamteua Patrick Qorro (marehemu). Wananchi walimwambia Dk Slaa aende chama chochote watamfuta na alipojiunga na Chadema mwaka huo, akashinda na hadi leo CCM ni chama cha upinzani Karatu.
Wanasiasa wengine mashuhuri waliowahi kumeguka CCM ni aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Chadema Dk Amani Wallid Kabouru ambaye leo ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma.

No comments: