CCM Dar yaikaba koo Tume ya Uchaguzi - LEKULE

Breaking

30 Jul 2015

CCM Dar yaikaba koo Tume ya Uchaguzi

Dar es Salaam.
Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusimamia kwa makini uandikishaji wapigakura jijini hapa ili wakazi wote wapate fursa ya kuandikishwa, ndani ya muda uliopangwa.

Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba aliwaambia wanahabari jana kuwa ufanisi katika uandikishaji utasaidia kumaliza idadi kubwa ya wakazi ambao bado hawajaandikishwa hadi sasa.

“NEC inatakiwa kuwa makini kukamilisha uandikishaji kwa kuongeza mashine na watendaji ili wakazi wengi wa Dar es Salaam waandikishwe,” alisema.

Kuhusu Lowassa

Simba alisema CCM haitatetereka na uamuzi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhamia Chadema.

Alisema uamuzi huo siyo wa kwanza, kwani Augustine Mrema aliwahi kuondoka CCM na kujiunga na upinzani.

Kauli ya kiongozi huyo imekuja siku moja tangu Lowassa na mkewe, Regina, waihame CCM na kujiunga na Chadema na kuahidi kuendelea na safari ya matumaini ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

“Lowassa alijiunga CCM kwa ridhaa yake, hakuna aliyemshurutisha na ametoka kwa ridhaa yake kwenda Chadema hakuna aliyemshurutisha. “CCM itabaki kuwa CCM zaidi ya hilo, lipi jipya?”
Simba alisema tishio kwamba Lowassa ataondoka na makada wengi wa chama hicho ni propaganda za kupuuzwa.

Jaji Lubuva alonga

Akizungumza na mwandishi wetu jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema muda wa kuandikisha wapigakura utaongezwa baada ya kujua idadi ya watakaosalia ifikapo mwisho wa kujiandikisha Agosti 31.

“Kwa sasa hatuwezi kusema tutaongeza siku ngapi, lakini ikifika siku ya mwisho tutajua watu wangapi wamebaki na hapo ndipo tutaongeza muda au la,” alisema Lubuva.
Alisema utaratibu wa kuanza uandikishaji kuanzia saa moja asubuhi hadi 12 jioni, unaweza kuongeza kasi ya uandikishaji na hivyo watakaosalia watapewa muda kulingana na idadi yao.

Waandikishaji wakaidi agizo la NEC

Licha ya NEC kutoa agizo kwa mawakala wa BVR kuanza kufungua vituo kuanzia saa moja asubuhi, badala ya saa mbili, baadhi ya mawakala katika vituo wamekaidi agizo hilo.
Jaji Lubuva alitoa agizo hilo juzi akiwataka mawakala hao kufungua vituo muda huo lengo likiwa kuhakikisha idadi kubwa ya watu wanaandikishwa.
Hata hivyo, agizo hilo lilionekana kupuuzwa na mawakala wa baadhi ya vituo ambao walifungua vituo hivyo kati ya saa mbili na saa tatu asubuhi.

Waandishi wetu walipita katika baadhi ya vituo na kukuta watu wakilalamikia suala hilo. Mmoja wa wananchi waliokuwa kwenye Kituo cha Shule ya Msingi Mivinjeni, Lekule Mollel alisema walifika kituoni hapo mapema, lakini kilifunguliwa saa tatu asubuhi na siyo saa moja kama inavyotakiwa.
Wakala wa kituo hicho, Malick Shaaban alikiri kuchelewa kufunguliwa kwa kituo hicho na kudai kuwa baadhi ya mawakala wanaishi mbali na eneo hilo.
Katika vituo vya Tabata, Temeke na Mbagala wananchi pia wamelalamik baadhi ya vituo kuchelewewa kufunguliwa tofauti na agizo.

Mkazi wa Tabata, aliyekuwa akijiandikisha kwenye Kituo cha Shule ya Sekondari Ari B, Tabata Kinyerezi, Elizabeth Mwijage alisema baadhi ya mawakala wa kituo hicho walipoulizwa juu ya hilo walidai hawakuwa na taarifa.

Licha ya kwamba walifungua saa moja, lakini uandikishaji ulianza saa tatu asubuhi kutokana na matatizo ya mashine kugoma kabla ya kuanza kazi.
“Tumefika hapa saa kumi na moja alfajiri tulivyoona wamewahi kufungua kituo tulifurahi tukijua uandikishaji utaanza mapema, lakini mashine zilichukua muda ilipofika saa tatu ndiyo mtu wa kwanza alianza kuandikishwa,” alisema Juma Pascal aliyekuwa Kituo cha Serikali ya Mtaa Kibondemaji B.


No comments: