Hotuba ya Bajeti Ya Wizara ya Ulinzi na JKT Kwa Mwaka 2015/2016 - LEKULE

Breaking

22 May 2015

Hotuba ya Bajeti Ya Wizara ya Ulinzi na JKT Kwa Mwaka 2015/2016

HOTUBA YA WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA MHESHIMIWA DKT. HUSSEIN ALI MWINYI (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA
KWA MWAKA 2015/16
UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Ulinzi na Usalama, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2015/16.

2. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aliyenijalia kuwa na uzima na afya njema na kuniwezesha kuwasilisha hotuba yangu ya bajeti kwa mwaka 2015/16. Aidha namshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuendelea kuniamini kuiongoza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Napenda kurejea ahadi yangu kwa Mhe. Rais na Watanzania wenzangu kuwa nitaendelea kutumia uwezo, nguvu na akili zangu zote kutekeleza majukumu yangu kwa haki, weledi, uaminifu, uadilifu na unyenyekevu wa hali ya juu ili kufanikisha malengo ya Taifa kwa ujumla na Wizara kwa hakika.

3. Mheshimiwa Spika, vile vile napenda kutumia fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wasaidizi wake Wakuu Kitaifa, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb) kwa kuiongoza nchi yetu vema na kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010-2015. Aidha napenda kumpongeza Spika wa Bunge hili Mhe. Anne Semamba Makinda (Mb), Naibu Spika Mhe. Job Yustino Ndugai (Mb) pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha vizuri shughuli za Bunge letu. Na kwa namna ya pekee, naungana na wenzangu kukupongeza Mhe. Spika kwa kuchaguliwa kwako kuwa Rais wa Jukwaa la Bunge la Nchi za Jumuiya yaMaendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Namwomba Mwenyezi Mungu azidi kuwapeni nyote baraka, hekima, busara na nguvu za kuendelea kuongoza Bunge hili katika kutekeleza majukumu yake mengi, mazito na nyeti. Pia napenda kutoa pongezi na shukrani za dhati kwa wananchi wa jimbo langu la Kwahani kwa kunipa ushirikiano katika kipindi chote cha miaka mitano niliyokuwa mwakilishi wao. Ni imani yangu kuwa tutayaendeleza mafanikio tuliyopata.

4. Mheshimiwa Spika , naomba kutumia nafasi hii kumshukuru tena Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama Mhe. Anna Margareth Abdallah (Mb) na Wajumbe wote wa Kamati hii Tukufu kwa kuendelea kunipa ushirikiano wa kutosha katika kuiongoza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kwa uhakika, Kamati hii imekuwa muhimili imara kwetu kwa kipindi chote kwani imesimamia, imeongoza, imeshauri, imefuatilia na imetembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara na hivyo kujionea yenyewe maendeleo na changamoto tunazokabiliana nazo. Ushauri na maelekezo ya Kamati yamechangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya Sekta ya Ulinzi na Usalama hapa Nchini. Na kwa uzito wa kipekee kabisa, na kwa niaba ya wapiganaji shupavu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, tunawapongeza na kuwashukuru kwa ziara yenu ya kihistoria mliyoifanya kuanzia tarehe 12-19 Aprili, 2015 kutembelea Wapiganaji wetu walioko nchini DRC. Ziara hiyo imeongeza ari na morali wa kazi kwa wapiganaji wetu wote.

5. Mheshimiwa Spika, ninaungana na wenzangu wote waliotangulia kuwapa pole wale waliopatwa na majanga, pamoja na kufiwa na ndugu, jamaa na wapendwa wao katika matukio mbalimbali yaliyotokea nchini yakiwemo mafuriko na ajali za vyombo vya usafiri yakiwemo mabasi ya abiria. Aidha, nachukua fursa hii kutoa salamu za pole kwako Mhe. Spika, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa kuondokewa na mpendwa wetu Mhe. Kapteni mstaafu John Damian Komba, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi. Naomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za Marehemu wote mahala pema Amina.

6. Mheshimiwa Spika , mwaka 2015 ni mwaka ambao Watanzania watahusika na masuala mengi muhimu yakiwemo kujiandikisha katika Daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Hivyo nikiwa kama mtanzania, na kwa kuzingatia kuwa Wizara yangu ni wadau wakubwa katika kufanikisha mustakabali wa Taifa letu, naungana na watanzania wengi wenye mapenzi mema na nchi yetu kuwaasa wananchi tushiriki kwa ukamilifu na kwa utulivu mkubwa katika kufanikisha masuala hayo muhimu kwa mustakabari wa Taifa letu.

7. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, napenda sasa kuchukua fursa hii kuwasilisha hotuba yangu ambayo kiujumla imejikita katika maeneo makuu yafuatayo: Malengo na majukumu ya Wizara; Utekelezaji wa Maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, Hali ya Ulinzi na Usalama, Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2014/15 na Mpango na Makadirio ya Bajeti kwa mwaka 2015/16.

MALENGO NA MAJUKUMU YA WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA
8. Mheshimiwa Spika, kama ilivyo katika Dira yetu, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inaendelea kuwa Taasisi iliyotukuka ya kulinda na kudumisha amani na usalama wa Taifa. Vivyo hivyo, tumeendelea kulinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya adui wa aina yoyote kutoka ndani au nje ya nchi na kuhakikisha kuwa Mamlaka ya nchi na maslahi ya Taifa letu yako salama sanjari na Dhima yetu.

9. Mheshimiwa Spika, katika kufanikisha Dira na Dhima zetu, malengo ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa yameendelea kuwa kama ifuatavyo:

i. Kuwa na jeshi dogo la Ulinzi wa Nchi lenye taaluma mpya, zana bora, vifaa vya kisasa na mawasiliano salama.

ii. Kuendeleza mazingira bora ya kufanyia kazi na makazi kwa kuimarisha yaliyopo na kujenga mapya.

iii. Kuimarisha tafiti za kijeshi katika mashirika ya Mzinga na Nyumbu na kuhawilisha teknolojia mpya.

iv. Kuendelea kuwajengea vijana wa kitanzania moyo wa uzalendo, ukakamavu, maadili mema na utaifa.

v. Kuimarisha utayari wa Jeshi la akiba.

vi. Kuhifadhi na kumiliki maeneo yake ya ardhi kwa ajili ya matumizi ya Jeshi.

vii. Kuendelea kudumisha amani na usalama kwa kushirikiana na nchi nyingine duniani.


10. Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo haya, Wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu yafuatayo:-

i. Uandikishwaji wa wanajeshi wenye sifa zinazohitajika kwa jeshi dogo
kwa ajili ya Ulinzi wa Taifa na kuwapatia mafunzo na mazoezi ya kinadharia na kivitendo.

ii. Kuwapatia wanajeshi makazi, zana, vifaa na vitendea kazi vipya, bora na vya kisasa.

iii. Kusimamia matunzo na matumizi mazuri ya zana, vifaa na vitendea kazi kwa ujumla.

iv. Kuimarisha mafunzo na mazoezi ya kijeshi ikiwa ni pamoja na shughuli za uendeshaji mafunzo ya ulinzi wa mgambo.

v. Kuboresha mitaala ya mafunzo ya JKT kwa vijana waliojiunga na mafunzo hayo kwa Mujibu wa Sheria au kwa utaratibu wa kujitolea ili iwaandae vijana hao kuwa wakakamavu, wenye nidhamu na kuwajengea moyo wa uzalendo na  mshikamano wa kitaifa katika kutekeleza shughuli za kujitegemea.

vi. Kuendeleza utafiti na uhawilishaji wa teknolojia za kijeshi na kuzalisha mali kupitia mashirika ya Mzinga na Nyumbu.

vii. Kuwezesha uzalishaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) kuwa
wa tija na faida itakayochangia katika uendeshaji wa shughuli za Jeshi la Kujenga Taifa.

viii. Kushirikiana na Mamlaka za kiraia pale inapobidi katika kukabiliana na majanga na dharura za kitaifa.

ix. Kuimarisha mazingira bora ya kuishi na kufanyia kazi na

x. Kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine duniani katika masuala ya kijeshi.

UTEKELEZAJI WA MAONI NA USHAURI WA KAMATI YA KUDUMU YA ULINZI NA USALAMA YA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

11. Mheshimiwa Spika, wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama ilipokaa na kujadili Makadirio ya Mapato, Mpango na Bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka 2014/15 ilitoa maoni, ushauri na maelekezo kadhaa kwa Wizara hii yaliyolenga kuboresha utendaji na utekelezaji wa majukumu yake. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa maoni, ushauri na maelekezo yaliyotolewa yamefanyiwa kazi na majibu yake yameainishwa katika Kiambatanisho Namba 1. Aidha, hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa mjadala huo pia zimezingatiwa katika mpango na bajeti ya mwaka 2015/16 ninayowasilisha leo hapa Bungeni.

HALI YA ULINZI NA USALAMA

(i) Ugaidi na Uharamia Duniani

12. Mheshimiwa Spika, vitendo vya kigaidi na uharamia vimeendelea kuwa tishio kubwa duniani. Mwelekeo wa matukio ya ugaidi hivi sasa ni matumizi ya mbinu na zana za kisasa ikiwemo teknolojia ya habari na  mawasiliano katika kufanikisha malengo yao bila kugundulika kiurahisi. Baadhi ya makundi ya ugaidi yanayoendesha harakati zake maeneo mbalimbali duniani ni pamoja na kundi la “Islamic State in Iraq and Syria (ISIS)”, Boko Haram, Al Qaeda na Al Shabaab. Makundi hayo yanaendesha kampeni za kurubuni na kuandikisha makundi ya vijana kutoka mataifa mbalimbali ili kujiunga nayo, hali ambayo inalifanya tishio la ugaidi kusambaa maeneo mengi duniani na kutokuwa na mipaka. Kutokana na ukubwa wa maeneo ya mipaka ya nchi yetu na kuwepo kwa mipenyo katika mipaka hiyo, upo uwezekano wa makundi ya kihalifu kutoka nje kuingia nchini na kufanya uhalifu ikiwemo kueneza itikadi zenye msimamo mkali (radicalization) pamoja na ugaidi. Tunaendelea kuwatahadharisha wananchi kuwa macho na kuyatolea taarifa matukio yanayotishia usalama wa nchi pindi yanapojitokeza.

13. Mheshimiwa Spika, Jeshi letu pamoja na kushirikiana vema na vyombo vingine vya ulinzi vya hapa nchini, pia limeshirikiana na majeshi mbali mbali katika kukabiliana na vitendo vya kigaida kwa kuimarisha doria na kuhakikisha eneo hilo la bahari linakuwa salama pamoja na vyombo vya usafirishaji baharini vinaendelea na shughuli zake bila tishio lolote.
Ushirikiano na majeshi mbalimbali umekuwa katika nyanja za mazoezi na operesheni za pamoja ambapo katika kipindi hiki, JWTZ lilifanya operesheni za pamoja katika Bahari ya Hindi na majeshi rafiki ya nchi za Kenya, Msumbiji na Afrika Kusini.

(ii) Hali ya Ulinzi na Usalama katika Nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati

14. Mheshimiwa Spika, hali ya Ulinzi na Usalama katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni shwari. Hata hivyo, ukanda huu umekuwa katika tahadhari ya kiusalama dhidi ya mashambulizi ya kigaidi kutoka kundi la Al Shabab la nchini Somalia. Ingawa kundi hili limekuwa likidai kulenga nchi zenye majeshi katika operesheni za Umoja wa Afrika nchini Somalia “The African Union Mission in Somalia (AMISOM),” mienendo yao imekuwa ikiashiria tofauti. Kwa msingi huo vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na raia wema vimekuwa macho na nyendo za wafuasi wa kundi hili. Pamoja na hayo, hali ya usalama wa nchi yetu kwa ujumla imeendelea kuwa shwari

15. Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo kumekuwepo na matukio machache yasiyokuwa ya kawaida na yenye dalili za uhalifu uliopitiliza (extended crime). Matukio haya yamepelekea mauaji ya askari wa JWTZ na wa Polisi na uporaji wa silaha. Naomba nichukue fursa hii kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba juhudi kubwa zimefanyika na zinaendelea kufanywa na vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama katika kukabiliana na wahalifu hao na mtandao wao. Tunawashukuru wananchi kwa ushirikiano wao katika kukabiliana na njama za uhalifu huu au kuwezesha wahalifu kukamatwa. Aidha, tunawaasa wananchi wote kuwa macho na maadui hao na kuwaomba waendelee kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kukabiliana nao.

16. Mheshimiwa Spika, vikundi vya uasi vyenye silaha vya “The Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR)”, “The Allied Democratic Forces” (ADF) na “The Lord’s Resistance Army” (LRA), vimesababisha hali ya usalama kuwa tete Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ingawa Kikundi cha FDLR kilitakiwa kujisalimisha mapema tarehe 02 Januari, 2015 kwa Majeshi ya Umoja wa Mataifa (“United Nations Organization Stabilization Mission in the DR Congo” – MONUSCO) hakikutekeleza kama kilivyotakiwa kwani hadi kufikia tarehe ya mwisho, ni asilimia 30 tu ya waasi hao walikuwa wamejisalimisha. Kutokana na hali hiyo taratibu za kukikabili Kikundi hicho zinaendelea chini ya Umoja wa Mataifa.

17. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa nchi ya Somalia na Sudan Kusini kumekuwa na hali tete ya Usalama hususan nchini Somalia kutokana na mapambano yanayoendelea baina ya majeshi ya AMISOM na kundi la Kigaidi la Al Shabaab. Aidha, hali ya uhusiano kati ya Serikali ya Sudan Kusini inayoongozwa na Rais Salva Kiir na kikundi kinachomuunga mkono Dkt. Riek Machar aliyekuwa Makamu wa Rais imeendelea kuwa tete. Hata hivyo, mazungumzo ya amani yanayoendelea yameanza kuonesha mwelekeo wa kupatikana ufumbuzi wa uhasama uliopo kati ya pande hizo mbili. Kwa upande wa uharamia wa baharini, hakuna matukio yaliyojitokeza katika mwaka 2014/15. Hata hivyo, vyombo vyetu vya ulinzi vinaendelea kufanya ulinzi mkali kwenye eneo letu.

(iii) Hali ya Usalama wa Mipaka

18. Mheshimiwa Spika, kufuatia juhudi kubwa zinazofanywa na vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na wananchi, majaribio ya ugaidi na matendo maovu ya biashara za madawa ya kulevya, uhamiaji haramu na ujambazi kwa ujumla yamepungua. Hali hiyo imepelekea hali ya mipaka yetu kuwa shwari. Kwa ujumla hali ya mipaka yetu imekuwa kama ifuatavyo:

(a) Mpaka wa Mashariki

19. Mheshimiwa Spika, katika mpaka huu wenye urefu wa km 1,424, nchi yetu inapakana na nchi za Kenya, visiwa vya Ushelisheli na Komoro na nchi ya Msumbiji. Hali ya usalama katika mpaka huu imeendelea kuwa shwari hakuna tukio lolote la kihalifu lililotokea katika kipindi hiki.

(b) Mpaka wa Kaskazini

20. Mheshimiwa Spika , katika mpaka huu wenye urefu wa kilomita 1,221 nchi yetu inapakana na nchi za Kenya na Uganda. Hali ya usalama katika mpaka huu kwa ujumla ilikuwa shwari. Hata hivyo, matukio ya uharibifu wa alama za mipaka (beacons) na ujenzi holela unaofanywa na baadhi ya watu waishio maeneo ya mipakani kwa lengo la kujipatia ardhi kwa ajili ya kilimo, malisho ya mifugo, biashara na ujenzi wa makazi yameendelea kujitokeza na hivyo kuwa changamoto kubwa kwa usalama wa nchi yetu.

(c) Mpaka wa Magharibi

21. Mheshimiwa Spika, mpaka wetu wa Magharibi una urefu wa kilomita 1,220. Katika mpaka huu Tanzania tunapakana na nchi za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Ingawa hali ya usalama wa mpaka huu kwa ujumla umekuwa shwari, matukio ya ujambazi wa kutumia silaha maeneo ya nchi kavu na katika Ziwa Tanganyika ambayo kwa sehemu kubwa yanafanywa na watu wenye silaha na baadhi yao wana uhusiano na vikundi vinavyohasimiana nchini DRC na wengine wakiwa ni masalia ya waasi kutoka nchini Burundi yameendelea kujitokeza. Katika ujambazi huo makundi hayo yamekuwa yakiwashambulia wavuvi na kuwanyang’anya fedha, bidhaa mbali mbali na vifaa vya uvuvi na hata kuwajeruhi.

22. Mheshimiwa Spika, mifano ya karibuni ni mwezi Desemba, 2014 ambapo majambazi wenye silaha za kivita wakiwa wamevaa sare za jeshi la nchi jirani waliwavamia na kuwapora wananchi wetu mali na fedha. Aidha, mwezi Novemba 2014, majambazi yenye silaha za kivita yaliwavamia wavuvi katika Ziwa Tanganyika na kuwapora mashine za boti zao na vifaa mbalimbali vya uvuvi na kumteka mvuvi mmoja wakampeleka nchi jirani na baadaye walimwachia na kumruhusu kurudi nyumbani. Matukio hayo ni kielelezo cha kuwepo kwa tishio la usalama katika mpaka wetu wa Magharibi. Hatua za kukabiliana na matukio hayo zimechukuliwa.

(d) Mpaka wa Kusini

23. Mheshimiwa Spika , mpaka wetu wa Kusini una urefu wa kilomita 1,536 ambapo Tanzania tunapakana na nchi za Msumbiji, Malawi na Zambia. Hali ya usalama katika mpaka huu imeendelea kuwa shwari. Pamoja na kwamba hatua ya mwisho ya kufikia usuluhishi mgogoro wa mpaka wetu na Malawi katika ziwa Nyasa bado haijafikia, hali ya kiusalama imeendelea kuwa shwari na wananchi wa pande zote wanaendelea na shughuli zao bila bugudha yoyote ya kiulinzi. Ombi letu kwa wenzetu wa Malawi ni kutulia na kuipa nafasi fursa ya usuluhishi wa mgogoro huo ikamilike.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2014/15

24. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15 Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilikadiria kukusanya mapato ya jumla ya shilingi 60,506,000.00 kutoka katika Mafungu yake matatu ya 38-NGOME, 39-JKT na 57- Wizara. Hadi kufikia mwezi Machi, 2015 Mafungu hayo yalifanikiwa kukusanya mapato ya jumla ya shilingi 47,268,778.00 sawa na asilimia 78.1 ya makadirio. Makusanyo hayo kwa kiwango kikubwa yamefanikiwa kama
ilivyokadiriwa. Hata hivyo kwa upande wa uchangiaji katika Mfuko wa Taifa, makusanyo 16 haya ni madogo kwa vile chanzo chake kikuu ni mauzo ya hati za zabuni, ambapo kwa sasa utangazaji huo unafanywa pia na GPSA na hivyo
kufanya mapato yake kupungua.

25. Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2014/15 Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iliidhinishiwa jumla ya shilingi 1,269,076,056,000.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Maendeleo katika Mafungu yake matatu. Kati ya fedha hizo, shilingi 1,020,076,056,000.00 zilitengwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 249,000,000,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo. Hata hivyo, kufuatia maelekezo ya HAZINA ya kurekebisha vitabu vya bajeti ya mwaka 2014/15, bajeti ya mafungu ilibadilika na kuwa shilingi 1,312,502,196,000.00 kukiwa na ongezeko la shilingi 43,426,140,000 sawa na asilimia 3.42. Kati ya fedha hizo shilingi 1,063,659,696,000.00 zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 248,842,500,000.00 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Mchanganuo wa bajeti hiyo kwa kuzingatia mafungu ya Wizara ni ufuatao:-

FUNGU                                                                          MATUMIZI
fungu                                   KAWAIDA                 MAENDELEO                                    JUMLA
NGOME                               839,635,388,000          12,000,000,000                     851,635,388,000
JKT                                     204,566,662,000            7,000,000,000                       211,566,662,000
WIZARA                            19,457,646,000               229,842,500,000                   249,300,146,000
JUMLA                             1,063,659,696,000          248,842,500,000            1,312,502,196,000


26. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2015, Wizara ilikuwa imepokea jumla ya shilingi 919,748,922,788.00 sawa na asilimia 70.07 ya bajeti. Kati ya fedha hizo shilingi 846,248,922,788.00 sawa na asilimia 92.0 zilitumika kwa shughuli za kawaida ikiwemo kulipa mishahara na posho mbalimbali muhimu. Kwa upande wa Matumizi ya Maendeleo, fedha zilizopokelewa ni shilingi 73,500,000,000.00 sawa na asilimia 29.53 ya fedha zote zilizoidhinishwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Mchanganuo wa Matumizi ya Kawaida na Maendeleo kwa Mafungu yote matatu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa hadi mwezi Machi, 2015 umeoneshwa katika Kiambatanisho Namba 2.

27. Mheshimiwa Spika, tathmini ya fedha zilizopokelewa inaonesha kwamba mwenendo wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida hususan fedha za mishahara na chakula kwa wanajeshi katika kipindi hicho kiujumla ulikuwa ni mzuri kwani fedha hizo zilipokelewa kulingana na makisio ya bajeti. Hata hivyo, fedha za Matumizi Mengineyo hazikutolewa kulingana na bajeti, kwani fedha zilizotolewa hadi Machi, 2015 zilikuwa asilimia 61.03 ya bajeti yake. Aidha, kwa upande wa shughuli za Maendeleo hadi kufikia mwezi Machi, 2015 fedha zilizotolewa zilikuwa asilimia 29.53 ya bajeti yake. Kiasi hicho ni kidogo sana ukilinganisha na mahitaji halisi yakiwemo kulipia madeni ya kimikataba ya ndani na nje. Hali hii pia imeathiri kasi ya upatikanaji wa vifaa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2014/15
MATUMIZI YA SHUGHULI ZA KAWAIDA

28. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilifanikiwa kutekeleza shughuli mbali mbali katika kufikia malengo iliyojiwekea. Shughuli hizo ni pamoja na kuwapatia stahili mbali mbali wanajeshi, watumishi wa umma na vijana walioko katika mafunzo ya JKT na kutoa huduma muhimu za chakula, tiba, sare, umeme, maji, simu na mafuta ya uendeshaji wa majukumu ya ulinzi.
29. Mheshimiwa Spika, majukumu ya kiulinzi yaliyotekelezwa katika kipindi hicho ni pamoja na kufanyika mafunzo na mazoezi ya kijeshi, mafunzo ya Ulinzi wa Mgambo, upatikanaji wa huduma za afya na tiba kwa maafisa, askari na wananchi, ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi na nchi nyingine, ushirikiano na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa, ushirikiano wa Jeshi na Mamlaka za Kiraia, Mafunzo ya JKT kwa vijana wa kujitolea na wa Mujibu wa Sheria.

(i) Mafunzo na Mazoezi ya Kijeshi

30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15 Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, limeendelea kutoa mafunzo na mazoezi kwa wanajeshi wake ili kulifanya kuwa imara na tayari muda wote kutekeleza majukumu yake ya kiulinzi. Aidha, Jeshi letu liliendelea kushiriki katika mafunzo na mazoezi ya pamoja na nchi marafiki. Miongoni mwa mazoezi hayo yalikuwa ni ya ZOEZI LA “URUSHAJI NDEGE VITA NA MAONESHO YA ZANA” katika Kamandi ya Jeshi la Anga lililofanyika Jijini Mwanza kati ya tarehe 23 – 28 Julai, 2014, ZOEZI LA “VALEDE lililotekelezwa na JESHI MAALUM” (Special Force), mwezi Agosti, 2014 nchini Angola, ZOEZI LA “USHIRIKIANO IMARA” lilifanyika nchini Burundi mwezi Oktoba, 2014, ZOEZI LA “SOUTHERN ACCORD” lililofanyika nchini Malawi mwezi Oktoba, 2014, ZOEZI LA UTULIVU AFRIKA lililofanyika nchini Tanzania mwezi Novemba, 2014 na ZOEZI LA MIAKA 50  YA JWTZ lililofanyika mkoani Arusha mwezi Septemba, 2014. Mazoezi ya aina hii mbali na kuliimarisha Jeshi kimedani pia, husaidia sana 20 kuboresha na kuimarisha mahusiano ya majeshi yetu na majeshi ya nchi nyingine.

(ii) Mafunzo ya Ulinzi wa Mgambo

31. Mheshimiwa Spika, mafunzo ya ulinzi wa Mgambo kwa wananchi yameendelea kutolewa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Katika kipindi cha mwaka 2014/15 JWTZ kwa kushirikiana na vyombo vya Usalama limeendesha mafunzo katika ngazi mbalimbali ambapo jumla ya wananchi 14,107 walifuzu. Hili ni ongezeko la wahitimu 623 sawa na asilimia 4.6 ukilinganisha na wananchi waliopata mafunzo hayo mwaka 2013/14. Kati yao waliofuzu mafunzo hayo, wanaume walikuwa 12,732 na wanawake 1,375. Naendelea kutoa wito kwa Viongozi wa ngazi mbalimbali kuhamasisha wananchi kushiriki katika mafunzo haya na pia kutoa huduma stahiki Mahsusi za hifadhi ya silaha na maeneo ya mafunzo.

(iii) Huduma za Afya na Tiba

32. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeendelea kutoa huduma za tiba kwa maafisa, askari, watumishi wa Umma, familia za wanajeshi na wananchi kwa ujumla. Huduma hizo zimekuwa zikitolewa katika Hospitali na Vituo vya tiba vya Jeshi hapa nchini. Aidha, huduma hizo zimeboreshwa baada ya kukamilika kwa mradi wa Ujenzi na ukarabati wa Chuo cha Sayansi za Tiba katika kambi ya Lugalo. Mipango yetu ni kukifikisha Chuo hicho katika hadhi ya kuwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi za tiba cha Muhimbili. Kwa sasa Chuo hicho kina uwezo wa kutoa elimu ngazi ya Stashahada ya juu kwa fani za udaktari msaidizi, uuguzi, maabara na Ufamasia. Mchakato wa kutoa elimu ngazi ya Shahada katika fani za unesi, maabara na afya ya jamii unaendelea vizuri.

33. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki, ajira 200 za wataalam wa tiba zimetolewa ili kukidhi mahitaji ya wataalam katika vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Aidha, katika juhudi za kuboresha miundo mbinu ya tiba kwenye vikosi vya Jeshi letu, miradi ifuatayo imekamilishwa ujenzi wa wodi mpya ya kisasa kwenye Hospitali Kuu ya Jeshi- Lugalo, ujenzi wa kituo cha uchunguzi (Diagnostic centre) katika Kikosi cha Jeshi Pemba, ujenzi wa jengo la X-Ray na Ultrasound katika Brigedi ya Songea, ujenzi wa jengo la maabara Kambi ya JKT Chita, upanuzi wa vituo vya utafiti wa ugonjwa wa malaria katika kambi za Jeshi la Kujenga Taifa Mgambo na Rwamkoma na ujenzi wa wodi ya Huduma ya Uzazi na Mtoto (Reproductive Child Health Care- RCH) Mwenge-Dar es Salaam. Pamoja na ujenzi wa wodi hii, kituo hiki kimepata msaada wa vifaa vya kisasa ikiwemo mashine ya kisasa ya kupimia Kansa ya matiti ambayo ilitolewa na Taasisi ya WAMA tarehe 27 Februari, 2015. Kwa nafasi hii, na kwa niaba ya Wizara naomba kumshukuru tena Mama Salma Kikwete kwa msaada wa mashine hiyo.

(iv) Ushirikiano wa Kiulinzi na Kijeshi na Nchi Nyingine

34. Mheshimiwa Spika, ushirikiano kati ya nchi yetu na nchi nyingine katika nyanja za kijeshi ni suala muhimu katika mustakabali wa ulinzi na usalama wetu. Kwa kuelewa hivyo, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeendelea kuwa na ushirikiano mzuri na majeshi ya nchi nyingine hususan katika mafunzo. Katika eneo hili, Jeshi letu limeendelea kupeleka maafisa wa ngazi mbalimbali kusoma katika vyuo vya kijeshi vya nchi marakifi zikiwemo China, Kenya, Uganda, Zambia, Rwanda, Afrika Kusini, Marekani, Ujerumani, Uingereza, Urusi na Falme za Kiarabu. Pia, maafisa kutoka katika baadhi ya Nchi hizi wapo hapa nchini katika vyuo vyetu vya kijeshi kwa mafunzo. Vyuo hivyo ni Chuo cha Maafisa Monduli (TMA), Chuo cha Ukamanda na Unadhimu (CSC) Arusha na Chuo cha Ulinzi wa Taifa (NDC) Dar es Salaam.

(v) Ushirikiano na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa

35. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, limeendelea kushirikiana na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa hususan katika Operesheni za ulinzi wa amani chini ya udhamini wa Umoja wa Nchi za Afrika (African Union) na Umoja wa Mataifa kama ifuatavyo: Kikosi kimoja cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kipo Darfur, Sudan maeneo ya Khor-Abeche na Meanawashe, kikosi kingine kipo Mashariki mwa DRC kama sehemu ya MONUSCO “Intervention Brigade (IB)” na Kombania mbili za Polisi Jeshi zipo nchini Lebanon. Aidha, Jeshi linao Maafisa wanadhimu na makamanda kwenye Operesheni za Ulinzi wa Amani nchini Sudan, Sudan Kusini, Ivory Coast, Lebanon, Central Africa Republic na DRC. Luteni Jenerali Paul Ignas Mella aliteuliwa kuongoza Majeshi ya Umoja wa Mataifa katika Jimbo la Darfur, Sudan chini ya “United Nation High Brid Mission in Darfur” (UNAMID). Jeshi letu pia lilipewa heshima ya kuteua mwakilishi maalum wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa Sudan Kusini, ambapo Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali alikabidhiwa jukumu hilo. Vikosi na maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania 24 waliopo kwenye operesheni za ulinzi wa amani wote wanaendelea vizuri na utekelezaji wa majukumu yao.

(vi) Ushirikiano wa Jeshi na Mamlaka za Kiraia

36. Mheshimiwa Spika, katika kusaidiana na Mamlaka za Kiraia katika shughuli mbalimbali za kiraia na utoaji wa misaada, JWTZ kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi lilishiriki kwa ukamilifu na kwa ufanisi mkubwa katika usambazaji nchini kote wa vitabu 2,500,000 vya masomo ya Sayansi na Hisabati vilivyotolewa msaada kutoka Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la USAID. Vitabu hivyo vilisambazwa kwa shule zote za Sekondari za Serikali Tanzania Bara kwa wakati na kuanza kutumika mwezi Januari, 2015 pale shule zilipofunguliwa. Nachukua fursa hii kuzipongeza Mamlaka za kiraia na taasisi zote kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa Jeshi wakati wa kutekeleza majukumu iliyopewa.

37. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia JKT imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza zoezi la uandikishaji wa wananchi ili kupatiwa vitambulisho vya Taifa. Katika mwaka 2014/15, jumla ya vijana 1,357 kutoka JKT walishiriki
katika zoezi la kuwaandikisha wananchi kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho hivyo. Kazi hiyo ilifanyika katika awamu mbili; awamu ya kwanza vijana 1,000 walishiriki katika zoezi hili kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro hususan katika Wilaya ya Kilombero kuanzia mwezi Agosti hadi Desemba, 2014. Awamu ya pili ambayo imehusisha vijana 357 inaendelea katika Wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani.

38. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2014/15, Jeshi letu lilishiriki katika kusafirisha msaada wa chakula (mahindi) na dawa uliotolewa na Serikali ya Tanzania kwa nchi ya Malawi kufuatia janga la mafuriko lililoikumba nchi hiyo mapema mwaka 2015. Jeshi kwa kutumia askari na magari yake lilifanikiwa kusafirisha jumla ya tani 1200 za mahindi na tani 60 za dawa za aina mbalimbali kwenda nchini Malawi katika mji wa Karonga. Kazi hiyo ilifanyika kuanzia tarehe 22 hadi 30 Machi, 2015 hivyo napenda kuungana na wananchi wengi kuipongeza Serikali kwa kitendo hicho. Aidha, nalipongeza Jeshi kwa kutimiza jukumu hilo kwa haraka, na pia katika kipindi hicho Jeshi lilisaidia katika ujenzi wa nyumba kwa wananchi wa Kahama walioathirika na mafuriko.

(vii) Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Vijana

39. Mheshimiwa Spika, mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa yameendelea kutolewa kwa vijana wa kujitolea na wale wa Mujibu wa Sheria wahitimu wa Kidato cha sita. Lengo la mafunzo hayo ni pamoja na kuwajengea uzalendo, ukakamavu, maadili mema, utaifa pamoja na kutoa stadi za kazi. Katika mwaka 2014/15 jumla ya vijana 40,082 walipatiwa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa, kati yao vijana 8,447 ni wa kujitolea na vijana 31,635 ni wa Mujibu wa Sheria. Mahudhurio hayo ya vijana wa mujibu wa sheria yameongezeka kwa vijana 15,632 ukilinganisha na vijana 16,003 waliohitimu mafunzo hayo mwaka 2013/14. Hata hivyo idadi hii bado ni pungufu ikilinganishwa na idadi ya vijana 41,000 waliostahili kujiunga na mafunzo hayo (wahitimu wa kidato cha sita). Miongoni mwa sababu zilizopelekea upungufu huu, ni kalenda ya awamu ya pili ya vijana kugongana na kalenda ya kuanza mihula ya Elimu ya Juu (mwezi Septemba). Wito wangu kwa vijana ni kushiriki mafunzo hayo kwani ni ya mujibu. Na kwa wale ambao hawakushiriki bila ridhaa yetu wataendelea kuwa kwenye orodha yetu ya vijana watoro. Wizara inatafuta uwezekano wa kuwawezesha JKT kuchukua kundi hilo la vijana kwa mkupuo mmoja wa Juni hadi Agosti ili kuwawezesha vijana wahitimu wa kidato cha sita waweze kuhudhuria mafunzo hayo na kuwahi muhula wa vyuo vya Elimu ya Juu.

40. Mheshimiwa Spika, dhima ya Jeshi la Kujenga Taifa ni kuwalea vijana wa kitanzania katika maadili mema, kuwajenga kinidhamu, kuwajengea uzalendo kwa nchi yao, kuwajengea ukakamavu, kufundisha na kuwapa ujuzi na stadi mbambali za kazi ili kuwaandalia mazingira mazuri ya kujiajiri mara wamalizapo mkataba wa mafunzo yao. Wakati wa kuandikishwa kujiunga na mafunzo hayo vijana hujaza na kusaini fomu ya mkataba maalum yenye masharti kwamba kijana awe tayari kurudi nyumbani mara amalizapo mkataba wake. Hata hivyo, tangu kuanza kwa utaratibu wa mafunzo hayo baadhi ya wahitimu wamekuwa wakiajiriwa na Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Taasisi binafsi kulingana na mahitaji ya vyombo hivyo. Ieleweke kuwa sio vijana wote wanaohitimu mafunzo hayo hupata ajira kwenye vyombo na Taasisi hizo. Napenda kutoa rai kwa vijana wanaopata mafunzo ya JKT wazingatie maarifa na ujuzi wanaoupata hususan wa stadi za kazi ili waweze kujiajiri badala ya imani inayoanza kujitokeza kwa baadhi yao kuwa kupitia JKT ni kigezo kikuu cha kuajiriwa Serikalini.

41. Mheshimiwa Spika, Mhe. Rais na Amiri Jeshi Mkuu alikwisha kutoa maagizo kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama la kuajiri vijana waliohitimu mafunzo ya JKT. Katika kutekeleza agizo hilo mwaka 2014/15 jumla ya vijana 8,590 waliajiriwa na vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa mchanganuo ufuatao: Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania liliandikisha vijana 6,531 kati yao wasichana ni 1,233 na wavulana 5,298; Jeshi la Polisi vijana 906 wasichana wakiwa 199 na wavulana 707; Usalama wa Taifa vijana 22 kati yao wasichana ni wanne (4); Jeshi la Magereza vijana 1,107 kati yao wasichana wakiwa 245 na wavulana 862; Jeshi la Zimamoto vijana 100 kati yao wasichana wakiwa 22 na wavulana 78 na TAKUKURU imeajiri vijana 24. Aidha, Taasisi na Makampuni binafsi kama Benki Kuu ya Tanzania, Baraza la Mitihani, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TANAPA, African Gold Mine na Geita Gold Mines kwa ujumla yameajiri vijana 2,214, tangu utaratibu wa mafunzo ya JKT yaliporejeshwa tena mwaka 2011 hadi sasa.

42. Mheshimiwa Spika, changamoto kuu ya utekelezaji wa mafunzo haya ni ufinyu wa bajeti unaosababisha kushindwa kugharamia huduma za mafunzo, kikamilifu na kushindwa kukarabati majengo na miundombinu katika makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa. Hata hivyo, baadhi ya changamoto zimeanza kutatuliwa kwa kutumia fedha kidogo zinazopatikana kutokana na vyanzo vya mapato ndani ya Jeshi la Kujenga Taifa.

(viii) Mapambano dhidi ya UKIMWI

43. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia kikamilifu mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa Maafisa, Askari, Vijana na Watumishi wa Umma na familia zao. Mapambano dhidi ya maambukizi haya yanaendelea kwenye Wizara na Taasisi zake. Baadhi ya mikakati ya mapambano hayo ni pamoja na kutoa elimu kwa wahusika wote kupitia mpango wa Elimu Rika kwa vikundi ili kujadili kwa undani namna ya kujikinga na maambukizi ya UKIMWI; kupitia mpango wa Tohara kwa vijana wa kiume kwenye makambi ya JKT. Mkakati mwingine ni upimaji wa hiari wa VVU kwa maafisa, askari, vijana na watumishi wa Umma na utoaji wa dawa za kufubaisha VVU na lishe kwa wale waliokwishaathirika.

(ix) Utawala Bora

44. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeendelea kutekeleza dhana ya utawala bora katika maeneo ya kazi kwa kushirikisha watumishi wake katika maamuzi, mapambano dhidi ya rushwa na utekelezaji wa sheria na kanuni za manunuzi ya Umma. Wafanyakazi hushirikishwa katika maamuzi kupitia wawakilishi wao kwa kutoa mawazo na changamoto mbalimbali zinazowakabili wakati wa vikao vya Baraza la Wafanyakazi. Pia, watumishi hushirikishwa kwenye maamuzi kupitia vikao vya Idara na Menejimenti. Katika kuhakikisha kuwa rushwa inadhibitiwa sehemu za kazi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeongeza uwazi katika mawasiliano pamoja na kuendelea kuwa na dawati linaloshughulikia malalamiko ya wafanyakazi. Vile vile, sheria ya manunuzi inazingatiwa wakati wa ununuzi wa vifaa vya ofisi na mahitaji mengine yanayohitaji zabuni. Mada ya Rushwa sasa ni agenda ya kudumu kwenye vikao vyote vya Baraza la wafanyakazi.

MATUMIZI YA SHUGHULI ZA MAENDELEO

45. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa shughuli za maendeleo hadi kufikia robo ya tatu ya Mwaka wa Fedha 2014/15 kwa ujumla haukuwa mzuri. Mafungu yote matatu yalipokea wastani wa asilimia 29.53 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kwa mapokezi hayo, Wizara yetu imeweza kutekeleza miradi ifuatayo; kuendeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 6,064 za makazi ya wanajeshi, kulipia madeni ya kimikataba, kukarabati majengo pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na makazi katika makambi na viteule vya JKT, ulipiaji fidia kwa baadhi ya maeneo yaliyotwaliwa kwa matumizi ya Jeshi, ujenzi wa Shule ya Mafunzo ya Awali ya Kijeshi Kihangaiko, kuendelea na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia silaha na zana na kuzindua mradi wa Mawasiliano ya Kimtandao katika maeneo ya Zanzibar, Pwani na Dar es Salaam.

(i) Ujenzi wa Nyumba na Makazi ya Wanajeshi

46. Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2014/15 nililitaarifu Bunge lako tukufu juu ya kuanza ujenzi wa nyumba 10,000 za kuishi wanajeshi vikosini. Katika ujenzi huo, tumeanza na awamu ya kwanza ya nyumba 6,064 ambapo ujenzi unaendelea vizuri na kwa kasi kubwa. Aidha, tarehe 20 Disemba, 2014 Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete aliweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa nyumba 552 zinazojengwa Monduli Mkoani Arusha kuwakilisha mradi wa ujenzi wa nyumba 6,064 katika mikoa tisa (9) hapa nchini. Mapema kabla yake , Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alizindua ujenzi wa nyumba 320 huko Pemba ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar tarehe 5 Januari, 2015.

47. Mheshimiwa Spika, sehemu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba hizi 6,064 umefanyika katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Hadi kufikia Januari, 2015 jumla ya nyumba 2,256 zilizokuwa zikijengwa mkoani Dar es Salaam zilikamilika. Uzinduzi rasmi wa nyumba hizo ulifanywa na Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe.Dkt Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 10 Januari, 2015 huko Gongo la Mboto ikiwa ni sehemu ya kukamilika kwa ujenzi wa awamu ya kwanza wa nyumba 6,064. Nyumba zote zilizokwisha kamilika zimeshakabidhiwa kwa JWTZ kwa ajili ya matumizi. Ujenzi katika vikosi mbalimbali vya JWTZ na JKT vilivyopo katika mikoa ifuatayo; Pwani (840), Arusha (792), Dar es Salaam (32), Dodoma (592), Kagera (144), Morogoro (616), Pemba (320), Kigoma (160) na Tanga (312) bado unaendelea.

(ii) Ununuzi wa Zana na Vifaa vya Kijeshi

48. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Serikali iliendelea kuliimarisha Jeshi kwa kulipatia zana na vifaa vya kisasa. Jeshi lilipokea zana na vifaa mbalimbali kwa ajili ya ulinzi wa anga, nchi kavu na majini. Kutokana na zana na vifaa hivyo Jeshi letu hivi sasa lina uwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu yake. Mpango huu wa ununuzi wa zana za kisasa na bora ni endelevu.

(iii) Shirika la Uzalishaji Mali la SUMAJKT

49. Mheshimiwa Spika, Shirika la Uzalishaji Mali la JKT (SUMAJKT) limeendelea kutekeleza shughuli zake katika misingi ya kibiashara. Shughuli kuu zinazoendeshwa na shirika hili kwa sasa ni katika nyanja za ujenzi uhandisi, viwanda, kilimo, biashara , utalii, na mradi wa uuzaji Matrekta na Kampuni ya Ulinzi kupitia SUMAJKT Guard Ltd.

50. Mheshimiwa Spika, SUMAJKT kupitia Idara ya ujenzi iitwayo “National Service Construction Department” inatekeleza miradi ya ujenzi katika sehemu mbalimbali nchini. Katika mwaka 2014/15 jumla ya miradi 39 ya ujenzi imetekelezwa. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa jengo la Kitega uchumi cha KKKT Kisukuru- Dar es Salaam, jengo katika Kanisa Katoliki Kristu Mfalme Tabata- Dar es Salaam, maabara katika baadhi ya shule za Sekondari zilizopo mkoani Kilimanjaro. Aidha, kupitia Idara ya viwanda na kilimo SUMAJKT lilifanikiwa kutengeneza samani mbalimbali katika kiwanda chake cha samani Chang’ombe-Dar es Salaam. Samani hizo ziliuzwa kwenye Idara na Taasisi za Serikali na watu binafsi.

51. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15 SUMAJKT kupitia sekta ya kilimo iliendelea na uzalishaji wa mbegu bora za mazao pamoja na uzalishaji wa mifugo. Aidha, Shirika lilishirikiana na Tanzania Investment Bank (TIB) kuboresha kilimo cha umwagiliaji cha zao la mpunga katika kikosi cha Chita kilichopo Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. Pia SUMAJKT lilishirikiana na “Tanzania Horticultural Association (TAHA)’’ ambacho ni Chama Cha Wazalishaji wa mboga na matunda kwa kutoa semina kwa watendaji katika vikosi kuhusu uzalishaji wa mboga, matunda, maua na viungo na namna ya kupata masoko ya ndani na nje ya nchi.

52. Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2014/15 SUMAJKT lilifanikiwa kuzalisha mahindi tani 1,160, mpunga tani 136, maharage tani 65.9, mafuta ya kula lita 2,162.9, mboga mboga na matunda tani 588.8. Aidha, katika mwaka huo huo jumla ya ekari 7,353 zililimwa kwa ajili ya uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula ukilinganisha na ekari 4,390 zilizolimwa mwaka 2013/14. Jumla ya ekari 2,337 zililimwa kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu bora ukilinganisha na ekari 1,913 zilizolimwa mwaka 2013/14 ikiwa ni ongezeko la ekari 424.

53. Mheshimiwa Spika, SUMAJKT imeendelea kuyauzia mbegu bora makampuni ya mbegu ya 35 Agricultural Seeds Agency (ASA), TANSEED, Tropical Seed Company Ltd, Southern Highland Seed Growers Ltd, Kibo Seed na SUBA Company iliyoingia nayo mikataba. Hata hivyo, katika utekelezaji wa mikataba hii kumejitokeza changamoto kwa makampuni hayo kutolipa madeni kwa wakati hali inayosababisha shirika kushindwa kufikia malengo yake. Hadi sasa jumla ya shilingi 908,716,976.00 hazijalipwa na makampuni hayo. SUMAJKT limeshachukua hatua za kisheria ya kuyafikisha Mahakamani makampuni inayoyadai. Aidha, SUMAJKT limesajili wakala wake wa mbegu ambalo linaitwa SUMAJKT SEED COMPANY LTD lenye usajili Namba 09818 ya tarehe 3 Februari, 2015 ili kuweza kusambaza kwa wingi na unafuu mbegu bora kwa wakulima.

54. Mheshimiwa Spika, katika kujipanua zaidi kibiashara SUMAJKT kupitia kampuni yake ya ulinzi ya SUMAJKT Guard Ltd. imeendelea kutoa huduma za ulinzi katika Idara za Serikali na sekta binafsi ikiwemo; vituo vya kuzalisha umeme vya Kihansi na Mtera mkoani Morogoro, TANESCO, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Wizara ya Fedha, CRDB, UBA, Migodi ya STAMIGOLD, Chuo cha madini Nzega na Chunya, TEMESA -Kivukoni na Busisi/Kigongo Mwanza na TPDC. Hadi sasa kampuni imeajiri walinzi 1,850, ikiwa ni ongezeko la walinzi 182

ukilinganisha na idadi ya walioajiriwa hadi kufikia Juni, 2014. Aidha, SUMAJKT imetenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji katika nyanja ya utalii ambapo shughuli zinazotarajiwa kufanyika ni pamoja na ujenzi wa mahoteli, vivutio sehemu za mapumziko, na kumbi za mikutano. Maeneo hayo yapo Makuyuni (Arusha), Kisiju (Pwani), Mbweni na Ndege Beach (Dar es Salaam.)

55. Mheshimiwa Spika,SUMAJKT limeendelea kuendesha na kusimamia mradi wa matrekta kwa niaba ya Serikali kuanzia mradi ulipozinduliwa tarehe 07 Oktoba, 2010 ukiwa na lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa kuongeza matumizi ya mashine za kisasa ili kuinua kipato cha wananchi, kuhamasisha matumizi bora ya matrekta, Power Tillers’ na zana mbalimbali za kilimo.

56. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi, 2015 SUMAJKT kupitia mradi huu lilifanikiwa kuuza matrekta 1,841 na zana 2,929 zenye thamani ya shilingi 65,550,428,807.00 kwa njia ya mkopo. Hata hivyo, ukusanyaji wa fedha za mkopo huo ambao ni utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi ulifikia shilingi 31,059,800,870.00 sawa na asilimia 47.4 ya thamani ya mali iliyouzwa. Awamu ya pili ya mradi huu ilianza Oktoba, 2013 ambapo ilihusisha ununuzi wa matrekta 268 kutoka India kwa thamani ya shilingi 7,046,245,600.00 . Awamu hii ya mradi inatarajia kukusanya jumla ya shilingi 8,551,692,701.48 baada ya mauzo yote. Hadi sasa jumla ya matrekta 232 yameshauzwa kwa wateja kwa thamani ya shilingi 7,609,603,059.28 sawa na asilimia 89. Napenda kuwakumbusha wadaiwa wote wa ndani na nje ya jengo lako tukufu kukamilisha malipo ya matrekta waliyokopa.

(iv) Shughuli za Shirika la Mzinga

57. Mheshimiwa Spika, kulingana na mpango mkakati wa Shirika wa miaka 15 kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2026, Shirika la Mzinga lina malengo yafuatayo:- kuendeleza uzalishaji wa mazao ya msingi kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi; kuanzisha kiwanda cha kuzalisha milipuko; kuanzisha kituo cha utafiti wa silaha za kijeshi na kusimika mfumo wa usalama wa kiwanda (electronic surveillance system). Katika mwaka 2014/15 Shirika la Mzinga lilikusudia kukamilisha ujenzi wa mkondo mpya wa risasi na ukarabati wa baadhi ya karakana na mitambo, kugharamia ujenzi wa maghala matatu mapya ya kuhifadhi silaha na kukamilisha uboreshaji wa mitambo ya uzalishaji awamu ya kwanza.

58. Mheshimiwa Spika, kutokana na ufinyu wa bajeti Shirika lilipata changamoto katika kutekeleza shughuli zake za msingi. Hata hivyo, kwa kutumia mapato madogo ya ndani Shirika limeendelea na uzalishaji katika mkondo wa risasi katika kaliba mbalimbali na ukarabati wa barabara za ndani na maeneo yanayozunguka Shirika. Aidha, shirika kupitia kampuni yake tanzu ya Mzinga Holding lilifanikiwa kutekeleza miradi mbali mbali ya kibiashara ikiwa pamoja na ukarabati wa jengo la Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, ujenzi wa vyumba vya maabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, ujenzi wa ‘box caravat’ Mabwepande katika Wilaya ya Kinondoni, ujenzi wa kiwanda cha maji ya kunywa na hosteli ya masista Jimbo Katoliki la Bukoba na ujenzi wa kituo cha afya Jimbo Katoliki la Kayanga.

(v) Shughuli za Shirika la Nyumbu

59. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15 Shirika la Nyumbu lilipanga kutekeleza shughuli zake za kuendeleza utafiti katika teknolojia ya magari na mitambo ya kijeshi, kuimarisha na kuongeza uwezo wa kuhawilisha teknolojia mbalimbali za utafiti na kukarabati miundombinu ya Shirika. Kutokana na ukosefu wa fedha za maendeleo, Shirika halikuweza kutekeleza shughuli zake za msingi. Hata hivyo, kwa kutumia mapato madogo ya ndani, Shirika
lilifanikiwa kufanya ukarabati mdogo wa nyumba za makazi na mitambo ya karakana ya Shirika; kununua vifaa vya TEHAMA na kukarabati mfumo wa umeme kiwandani.

(vi) Mtandao wa Mawasiliano Jeshini

60. Mheshimiwa Spika, Wizara inatekeleza mradi wa Mawasiliano Salama ya Kujitegemea Jeshini (Independent Secured Mobile Communication Network). Hadi kufikia Machi, 2015 jumla ya minara 131 ilisimikwa Tanzania Bara na Visiwani na vituo (Control Centre) viwili kwa ajili ya kuendesha na kusimamia mawasiliano hayo vilishajengwa Dar es Salaam na Dodoma. Mtandao huu umefanyiwa majaribio wakati wa sherehe za maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar tarehe 12 Januari, 2015 ambapo mawasiliano ya kimtandao yaliweza kupatikana katika maeneo ya Zanzibar, Pwani na Dar es Salaam. Kazi ya kuunganisha maeneo mengine ya nchi kwenye mtandao huo inaendelea. Kwenye minara iliyokwishasimikwa hatua za kufikisha umeme wa TANESCO zinachukuliwa ili kuepuka gharama za kutumia jenereta kuendesha minara hiyo.

(vii) Kudhibiti Uvamizi wa Maeneo ya Jeshi, Upimaji na Ulipaji Fidia

61. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, itaendelea na utaratibu wake wa kulipatia JWTZ na JKT maeneo ya 40 ardhi kwa ajili ya matumizi yao. Matumizi hayo ni kwa shughuli muhimu kama maeneo ya mazoezi ya Kijeshi na medani, shughuli za ujenzi na shughuli za miradi zinazofanywa na JKT na mashirika ya Mzinga na Nyumbu. Pamoja na mahitaji hayo kuwa makubwa upatikanaji wake hutegemea fedha hususan za fidia. Kama nilivyoahidi, mwaka 2014/15 tumeweza kulipa fidia kwa maeneo ya Mataya – Bagamoyo, Mwakidila – Tanga, Mwantini – Shinyanga, Mahongole – Makambako na Kasanga – Rukwa na upimaji wa maeneo ya Ilemela – Mwanza, Mahungu na Ntyuka- Dodoma. Katika kipindi hiki Wizara haikuweza kulipa fidia kwa baadhi ya maeneo tuliyokusudia katika mwaka 2014/15 kutokana na uhaba wa fedha. Maeneo hayo ni pamoja na Kimbiji – Temeke na Tanganyika Packers – Arusha.

62. Mheshimiwa Spika , zoezi la kupima na kulipa fidia maeneo ya Jeshi ni endelevu, ambapo mwaka 2015/16 upimaji na kulipa fidia unategemea kufanyika kwa maeneo ya kilima cha Ilemela, Lukobe na Kigongo Ferry – Mwanza, Kimbiji – Temeke, Ras Nondwa – Kigoma, Ronsoti – Tarime, Tanganyika Packers – Arusha na Kaboya – Muleba. Kimsingi maeneo ya Jeshi yaliwekwa mbali na mijini na vijijini kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kistratejia, usalama na uhalisia wa shughuli za kijeshi (military manouvres). Pamoja na maeneo ya Jeshi kuwa mbali na shughuli za kiraia, kumekuwa na mienendo ya baadhi ya wananchi kuvamia maeneo hayo kwa visingizio mbalimbali. Wito wangu kwa wananchi waache tabia ya kuvamia maeneo ya Jeshi kwani pamoja na ukweli kuwa ni hatari lakini pia wanakwaza shughuli za Jeshi.

CHANGAMOTO ZA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KATIKA MWAKA 2014/15

63. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali lakini kubwa ikiwa ni kupata kiwango kidogo cha fedha ukilinganisha na bajeti halisi. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara iliomba shilingi 708,731,094,124.00 kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vyake, lakini kiasi kilichoidhinishiwa ni shilingi 248,842,500,000.00 tu sawa na asilimia 35.1 ya mahitaji hayo. Hali hii kwa kiasi
kikubwa imekuwa ikiathiri utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Maendeleo ya Jeshi, mfano kushindwa kulipa mikopo mbalimbali ya kimikataba.

64. Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine inayoikabili Wizara ni mtiririko wenyewe wa fedha kutoka Hazina ambao hauzingatii Mpango Kazi wa Wizara. Aidha, fedha hutolewa zikiwa pungufu na bila kuzingatia ratiba ya utekelezaji. Hali hii inasababisha shughuli za Wizara hususan za maendeleo kutotekelezwa kama ilivyopangwa na hivyo kushindwa kukamilisha ujenzi wa majengo na miundombinu katika makambi, kukwama kwa shughuli za viwanda, karakana na shughuli za utafiti. Aidha, Wizara inashindwa kutoa huduma na mahitaji muhimu kwa wanajeshi na watumishi wa umma.

MPANGO WA MWAKA 2015/16

65. Mheshimiwa Spika, mpango na malengo ya Wizara ya Ulinzi na JKT katika mwaka 2015/16 ni kuendelea kuimarisha uwezo wa kulinda mipaka ya nchi yetu pamoja na kuimarisha mazingira ya amani na utulivu na nchi nyingine duniani, hususan na nchi jirani. Ili kufikia mpango na malengo hayo, Wizara imekusudia kutekeleza majukumu yafuatayo:-
a. Kuendelea kuliimarisha na kuliongezea uwezo Jeshi katika utendaji kivita kwa kulipatia vifaa na zana bora za kisasa pamoja na kutoa mafunzo stahiki kwa wanajeshi dhidi ya adui wa ndani na nje.
b. Kulijengea Jeshi mazingira mazuri ya kufanyia kazi na makazi ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za kuishi wanajeshi katika makambi na kuimarisha upatikanaji wa huduma na mahitaji ya msingi kama vile chakula, tiba, sare, usafiri, maslahi na stahili kwa wanajeshi na watumishi raia.
c. Kuimarisha uwezo wa Jeshi katika utafiti na kuendeleza teknolojia kwa madhumuni ya kuzalisha bidhaa na huduma kwa ajili ya matumizi ya kijeshi na kiraia hapa nchini na nje ya nchi.
d. Kuendelea kuwapatia vijana wa Kitanzania mafunzo ya uzalendo, umoja wa Kitaifa, ukakamavu na kuwaandaa katika uzalishaji na stadi mbalimbali katika makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa.
e. Kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi na nchi nyingine duniani kupitia Jumuiya za Kimataifa, Kikanda na ushirikiano na nchi moja moja. Ushirikiano wa Kikanda unahusisha ushirikiano wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa nchi za Afrika (AU).

SHUKRANI

66. Mheshimiwa Spika, kabla sijahitimisha Hotuba yangu napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wafuatao kwa michango yao katika maandalizi ya taarifa hii ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu; Katibu Mkuu Bw. Job D. Masima, Naibu Katibu Mkuu Bi. Mwintango Rose Shelukindo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis A Mwamunyange, Mnadhimu Mkuu Luteni Jenerali Samuel A Ndomba, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Raphael M Muhuga, Wakuu wa Kamandi za Jeshi la Nchi Kavu Meja Jenerali Salum M Kijuu, Jeshi la Anga Meja Jenerali Joseph F Kapwani na Jeshi la Wanamaji Meja Jenerali Rogastian S Laswai, Meneja Mkuu wa Shirika la Mzinga MejaJenerali Dkt. Charles N Muzanila na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumbu Brigedia Jenerali Anselm A Bahati.

67. Mheshimiwa Spika, pia napenda kuwashukuru Wakuu wa Idara na Vitengo (Makao Makuu ya Wizara), Wakuu wa Matawi (NGOME), Wakuu wa Idara (Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa), Maafisa, Askari na Watumishi wa Umma wa Wizara kwa kunipa ushirikiano katika kufanikisha majukumu ya Wizara. Aidha, naishukuru Kamati ya Wizara iliyoandaa hotuba hii na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha hotuba hii kwa wakati.

68. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mnyimi wa fadhila endapo sitawashukuru Wahisani mbalimbali waliotoa michango yao kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha maendeleo ya Jeshi. Wahisani hao ni pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, ambao wameshiriki katika upanuzi wa uwanja wa ndege Ngerengere na ujenzi wa nyumba za makazi ya wanajeshi 6,064 kupitia mkopo nafuu kutoka Benki ya EXIM China. Vilevile naishukuru Serikali ya Ujerumani ambayo imeshiriki katika ujenzi wa vituo vya afya vya Kanda, ukarabati na uboreshaji wa karakana kuu ya Jeshi Lugalo na uboreshaji wa Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo. Nazishukuru pia nchi zifuatazo kwa ushirikiano tuliokuwa nao katika nyanja za ulinzi pamoja na mafunzo. Nchi hizi ni Afrika Kusini, Bangladesh, Burundi, Canada, China, DRC, Ghana, Falme za Kiarabu, Indoneshia, Kenya, Marekani, Msumbiji, Misri, Namibia, Nigeria, Rwanda,Uganda, Ujerumani, Uingereza, Urusi, Zambia na Zimbabwe.

69. Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu wa pekee na kwa kupitia Bunge lako Tukufu naomba kuwasilisha salamu za pongezi maalum za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa wanajeshi wote kwa kufanikisha maadhimisho ya miaka 50 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania yaliyofanyika Arusha mwezi Septemba, 2014. Aidha, kwa kumalizia na kwa niaba ya wanajeshi wote namshukuru sana Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa uongozi wake uliotukuka kwa kipindi cha miaka kumi. Mhe. Rais atakumbukwa na kuenziwa vizazi na vizazi hususan kwetu sisi wanajeshi. Ahadi yetu kwake ni kuwa tutaendelea kusimama imara, kupokea na kutii amri na maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu.

MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA BAJETI YA MWAKA 2015/16

(i) Makadirio ya Mapato

70. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Taasisi zake haina vyanzo vya uhakika vya mapato vinavyoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukusanyaji wa maduhuli. Hali hii inasababishwa na majukumu ya msingi ya Wizara hii. Chanzo kikuu cha mapato ni makusanyo ya mauzo yanayotokana na nyaraka za zabuni, suala ambalo kwa sasa linashughulikiwa pia na GPSA.

71. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/16 Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inatarajia kukusanya jumla ya shilingi 72,606,000/= katika mchanganuo ufuatao:-
Fungu 38 – NGOME   shilingi       11,601,000.00
Fungu 39 – JKT           shilingi       50,003,000.00
Fungu 57 – Wizara      shilingi       11,002,000.00
(ii) Matumizi ya Kawaida na Maendeleo

72. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inaomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 1,716,301,362,000.00 kwa ajili ya Matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo ili iweze kutekeleza majukumu yake katika mwaka 2015/16. Kati ya fedha hizo shilingi 1,477,163,404,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 239,137,958,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo. Mchanganuo kwa kila Fungu ni ufuatao:-

Fungu 38 – NGOME
Matumizi ya Kawaida         shilingi       1,163,083,841,000.00
Matumizi ya Maendeleo     shilingi       12,000,000,000.00
Jumla                                    shilingi       1 ,175,083,841,000.00

Fungu 39 – JKT
Matumizi ya Kawaida         shilingi      292,296,992,000.00
Matumizi ya Maendeleo     shilingi      7,000,000,000.00
Jumla                                    shilingi       299,296,992,000.00

Fungu 57 – Wizara
Matumizi ya Kawaida         shilingi      21,782,571,000.00
Matumizi ya Maendeleo    shilingi      220,137,958,000.00
Jumla                                   shilingi       241,920,529,000.00

MWISHO

73. Mheshimiwa Spika, hotuba hii inapatikana pia katika tovuti ya Wizara
(www.modans.go.tz). Naomba kutoa Hoja.

No comments: